“Nilikuwa nikiishi nyumba ya nyasi, lakini sasa nimejenga ya bati kwa Sh6 milioni, nimefanikiwa kununua nyumba ya biashara mjini Iringa, kwa Sh50 milioni, namudu kuwasomesha watoto wangu shule nzuri na nina mtaji wa kuendeleza kilimo cha kisasa,” anasema Mgimba. Mara yangu ya kwanza kukutana na Mgimba, ilikuwa miezi miwili iliyopita katika soko kuu la Manispaa ya Iringa wakati akishusha mzigo wake wa nyanya huku, baadhi ya wafanyabishara wakigombea nyanya hizo. Kwa sababu nilikuwa nikifuatilia bei za mazao sokoni, sikuona tabu kusogea karibu na eneo hilo kujua bei ya nyanya.“Tenga moja ni Sh18,000, bei ndogo tofauti na thamani ya nyanya zenyewe. Haina haja ya kuhifadhi kwenye friji kwa sababu zinaweza kukaa siku 40 bila kuharibika baada ya mavuno,”anasema Mtokambali wakati akiwavutia wateja wake, ambao pia walionekana kuhitaji mzigo huo licha ya bei kuwa juu. Niliamua kumvuta pembeni, Mzee huyo kujua ukweli wa matangazo yake na alisisitiza: “Njoo shambani kwangu uvune nyanya kadhaa, na kuzifanyia utafiti uhakikishe jambo hili.”
Baada ya kauli hiyo nilinunua nyanya kadhaa ambazo nilizihifadhi kwa siku 30, huku zikionekana kutoharibiika na baadaye niliwasiliana naye kupata maelezo zaidi. “Nilipewa mafunzo ya kilimo cha nyanya, nikajiunga kwenye mtandao wa wakulima wa Nyanya Wilayani Iringa na baadae nikaelekezwa mbegu bora ya nyanya ambazo baada ya mavuno zinaweza kuhimili muda mrefu bila kuharibika,” anasema. Wakati wenzie wakiuza tenga moja la nyanya Sh6,000 hasa wakati wa msimu, Mgimba anauza Sh18,00, lakini wakati nyanya zinapokuwa chache sokoni anauza tenga moja Sh20,000 mpaka Sh25,000 huku wenzake wakiuza Sh10,000 mpaka 12,000. Katika msimu huu wa Kilimo, anasema tayari amevuna tenga 396 za nyanya ambazo ameuza kati ya Sh18,000 mpaka Sh25,000 kwa tenga moja na kupata Sh12 milioni.“Nimevuna tenga 396 na bado naendelea kuvuna kwa sababu uvunaji wa nyanya tofauti na mazao mengine. Mpaka sasa nimevuna mara tisa, bado kama mara tatu nipate zaidi ya tenga 100 zilizosalia kwenye eneo hili.
“Eneo nilililovuna nyanya hizi ni nusu eka ya kwanza, lipo eneo lingine ambalo sijaanza kwa vile nyanya bado hazijakomaa,”anasema.Kutokana na ina ya nyanya anazolima, soko la nyanya hizo linapatikana kirahisi kwa vile wafanyabishara wengi wamekuwa wakizipenda kutokana na sifa ya kukaa muda mrefu bila kuharibiika.Kuna wakati wateja wamekuwa wakimfuata shambani, na wakati mwingine amekuwa wakiwapelekea wateja hao nyanya.
Nilianza kulima baada ya kustaafu kazi
“Siku nilipopewa barua ya kustaafu kazi, sikudhani kama ningeweza kuendeleza maisha yangu, moyo wangu ulitawaliwa na fikra za kuajiriwa, nilikata tamaa, nikakonda kwa mawazo, nikiamini huo ndio ulikuwa mwisho wangu wa mafanikio,” anasema Mgimba. Kwa maana hiyo, ajira ilikuwa ni kila kitu katika maisha yake hivyo hakuwahi kuamini, kama anaweza kuendesha maisha kwa njia nyingine yoyote. Ugumu wa maisha, ulisababisha akimbilie kijijini ambako, alifungua mashamba ya mahindi. “Ilifikia hatua sikuwa na uwezo wa kulipa pango la nyumba, kununua chakula wala kuwalipia ada wanangu. Hapo ndipo niliamua kurudi kijijini kuanza maisha mapya ya kilimo mbacho siku zote sikukipenda kwa sababu wakulima wengi niliowaona walikuwa maskini,” anasema.
Kilimo cha mahindi hakikumletea maendeleo kwani hata baada ya kuvuna mazao mengi, hakuweza kuuza kwa bei nzuri kwa sababu wakulima wengi walikuwa wakilima mahindi na soko lilikuwa la kubahatisha. Miaka mitano iliyopita, Mgimba alibadili mazao yake na kuanza kulima nyanya, baada ya jirani yake kulima zao hilo na kumletea nafuu ya maisha. Pamoja na hayo elimu duni kuhusu kilimo cha nyanya, kilisababisha apate mavuno kidogo tofauti na matarajio yake. Mbali na hayo wakulima wa nyanya katika kijiji hicho wamepata mafunzo kutoka kwa Muungano wa Wajasiriamali vijijini (Muvi).Baada ya mafunzo hayo, wakulima hao walihamasishwa kuanzisha umoja wao ili iwe rahisi kuendelea kupatiwa mafunzo sambamba na pembejeo ikiwamo mbegu ambazo zilikuwa tatizo kwa.
“Huko ndiko nilikopata elimu ya kutosha ambayo leo hii imenifikisha hapa nilipo. Wamekuwa wakituunganisha na kampuni zinazozalisha mbegu za kisasa kama,” anasema. Anasema yupo katika mikakati ya kununua gari la mizigo aina ya fuso, ambalo atalitumia kusafirisha nyanya hizo mpaka sokoni tofauti na sasa amekuwa akitegemea zaidi magari ya kukodi

Mgimba ambaye ana mke na watoto wanne anasema anakabiliwa na tatizo la mbegu ambazo wamekuwa wakinunua Sh180,000 kwa gramu 30 na mbolea.
Kauli ya Muvi
Mratibu wa Muvi, Mkoa wa Iringa, Willima Mwaikambo anasema wamefanya utafiti kuhusu nyanya zinazozalishwa na Mgimba, na wamebaini zinakaa zaidi ya siku 35 katika eneo lenye hali ya hewa ya kati na siku 40 kwa eneo lenye baridi.
Anasema wamechukua nyanya hizo na kuzisafirisha jijini Dar es Salaam ambako wameanza kutafiti ili kujua, zikiwa sehemu ya joto zinaweza kuhimili muda gani bila kuharibiika. Anasema kwa sasa wametafuta kampuni ya Mosanto, kutoka Kenya ambayo imekuwa ikizalisha mbegu za Edeni, ambazo sifa yake kubwa ni kuhimili muda mrefu bila kuharibiika na kwamba limekuwa likimsaidia mkulima kutafuta soko kwa wakati bila hofu ya nyanya zake kuharibika. Jitihada kubwa za Muvi zimejikita kuhakikisha wakulima wa zao hilo wanalima kilimo cha kisasa na chenye tija ambacho kitaweza kuwakwamua kiuchumi. Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Getrude Mpaka anasema kulingana na taarifa za maendeleo ya kilimo mkoani Iringa na Shirika la Kilimo Duniani (FAO), zaidi ya asilimia 70 ya Nyanya zinazolishwa nchini Tanzania, zinazalishwa mkoani Iringa.
Kilimo cha nyanya kinatoa ajira kwa zaidi ya kaya 35,000, mkoani Iringa na kwamba soko lake halipo tu ndani ya Tanzania bali lipo pia katika nchi zingine za Afrika kama Kenya, Comoro na Congo DRC.

No comments:
Post a Comment